Kuna dereva bajaj namkubali sana, anafanya kazi kwa bidii, ana smile kila siku nnapo muona,

 hali ikiwa nzuri hali ikiwa mbaya ni mtu mwema sana. Ila bosi wake hamthamini, dunia haimthamini. Bajaj yake anayotumia ni mbovu, inapata matatizo kila siku, haijalipiwa baadhi ya vibali kwahiyo anakamatwa na kulipa fine ndogo ndogo hapa na pale, juhudi zake zinaishia kuonganisha nyaya na kucheza na bolti ili bajaj iendelee kufanya kazi apate hela ya kwake kujimudu na maisha na pia apeleke hela kwa bosi wake.
Hii ndio dunia tunayoishi kwa sahivi, mtu anazaliwa kwenye hali flani ya maisha na kutokana na mifumo ya kila siku, maisha yanazidi kumuweka chini, fanya kazi kwa bidii utafika sehemu nzuri wanakwambia, ila hao wanaosema hivyo hawajui ni mambo mangapi watu wenye hali duni wanakabiliana nayo kwenye maisha ya kila siku, huyu anaeendesha bajaj anashindwa, ama ina muwia vigumu sana kuwekeza kwenye kitu chochote cha kujiendeleza kama hamna mfumo wa kumsaidia, anashindwa kuwekeza kwenye afya, kwenye kujiendeleza kimasomo, kwenye akiba, anakubaliana tu na hali ya maisha kila siku.
Hii hali inanigusa sana na kunikumbusha kipindi ambacho nipo nahangaika kuweza kumudu maisha, somo ambalo nilijifunza juu ya maisha, ni kuweza ondoa uwoga. Kipindi hiko bado kijana mdogo na najifunza mengi, nilifanikiwa kuweza ku master uwoga inapokuja kwenye hali ya maisha, haswahaswa kwenye kufanya kazi kwa watu ambao hawathamini uwepo wako.
Nakumbuka nikiwa nna miaka 18 hivi, mishemishe za hapa na pale zikawa hazileti mafao, nkaamua nijikite kwenye ajira kwa kipindi kidogo, kuna kazi nikaitwa interview, nikaipita, offer wakanipa laki tatu, nkawa sina pengine pa kwenda hata kama hiyo hela ilikua ndogo sana, nikaona ngoja nijaribu hata miezi miwili mitatu niweze simama kisha niache, nkamwambia bosi (alikua muhindi huyu), angalau apandishe ifike tano, mi ntapiga kazi hajawahi ona, akakataa, akasema tuanze tu, mshahara utapanda.

Day 1. Hii kazi ilikua kama graphics designer/web designer. Na kama task ya kwanza niliyopewa ni kuitengenezea website kampuni flani hivi, kubwa tu. bosi akasema “hii website tumejaribu ifanya miezi miwili hatuja maliza, umeanza kazi leo, hii ndio itakua task yako”, ikamilishe hii website, tuone uwezo wako. Nikaichukua hiyo kazi mida ya mchana saa nane hivi, kichwani mwangu nikawaza ngoja nimuoneshe huyu mtu kwamba mimi ni asset kubwa sana akinitumia vizuri atatengeneza hela zaidi, nikakesha na hiyo website, design, code, design code, usiku hadi saa tisa flani hivi nikaimaliza.

Day 2. Nikafika ofisini. nmechelewa kama nusu saa hivi siku ya pili tu, mmoja wa wafanyakazi wenzangu, anavaa miwani huyu jamaa (jina simkumbuki, ila atarudi tena kwenye simulizi, tumuite allen), allen akasema “uwe unawahi michael, bosi akijua unachelewa itakua ishu”, kwa mtu yoyote anaenijua anajua mimi sinaga kuwahi ofisini kwa mtu, kama kazi namaliza on time, sitojisumbua kukimbia asubuhi ili nije kukaa tushangaane tu. Anyway, nikafika, nikakaa, nkaweka begi chini, nkafungua laptop na kumpelekea bosi aone website, aisee bosi aliipenda sana. Mda mwingi sana huyu bosi huwa hana tabasamu yupo serious tu, ila asubuhi hii aka tabasamu kidogo. Akaniambia niiweke mtandaoni ili client aone, nikaenda nikaiweka nikaenda kukaa chini kwenye meza nikafungua laptop na kufanya mambo mengine, nkashangaa watu wananiangalia ambao tupo ofisi moja, ghafla allen akaitwa ofisini.

Allen alipotoka ofisini akaja karibia na meza yangu na kuniita turudi ofisini kwa bosi, tukafika kwa bosi. Bosi akanisifia kidogo, kisha akasema “enhee, michael tupige kazi sasa, kuna hizi website mbili zingine tuzifanye, wateja tutapata wengi”, akaendelea kuongea mengine. Mi nikakaa na kumsikiliza tu, ila moyoni mwangu nikajua kwa kumuangalia tu kwamba huyu mtu hato kuja kujua thamani yangu, na nini ambacho naweza kumfanyia kwenye biashara yake, nkaona mimi sito jifunza chochote kwenye hii kampuni zaidi ya kutumika, bosi anaongea mambo mengi hapa ila simsikii mi nawaza tu nini ntafanya.

Maisha ni mafupi na wengi wetu tunafanya mambo kwa ajili ya uwoga, tunaogopa. Mi nilikua na uwoga kama watu wengi tu, hii kazi haitonisaidia kwa kitu chochote kingine zaidi ya hela kidogo tu, ambazo zitaishia kwenye nauli, chakula, na umeme. sitowekeza, sitoongeza ujuzi, sitopanda kwenye ngazi ya mafanikio ya maisha haya, akili haitokua, haito nichallenge, lakini nataka niifanye kwa kua naogopa tu kuja kuishiwa hela, na kukosa hela za kula, au za kulipia kodi sehemu ninayo kaa, na huu owoga ni wa kweli kwa kua maisha ya sasa yanakulazimu kufanya chochote ili kutengeneza kipato, bila hivyo ukiumwa, ukiwa na njaa au ukikosa sehemu ya kukaa, ni juu yako, kwahiyo huu ni kama mtego flani.

Siku ya pili kazini hapo, siku inaishia, nikawaza ntafanya nini, kwa maana nahitaji kazi kwa sahivi, ila mazingira ya kazi siyapendelei, na bosi hatutopatana kabisa, nkaona ngoja nikalale tu, kesho nikiamka ntajua nini cha kufanya, usiku huo sijui niliota nini, maana siku inayofuata nikaacha kazi, hata nauli ya kwenda ofisini kwa siku hii ya tatu nilikua sina, nikaomba sh elfu mbili kwa jirani.

Day 3. Nakumbuka hii siku kama ilikua jana hivi. Hamna siku ambayo niliamini kwamba nafanya kitu sawa kama siku hii. Nikajiandaa nikachana nywele, nikavaa pair yangu moja ya kiatu na kujibeba kwenda hadi ofisini. Nikafika nikakaa, kama kawaida mi ndio wa mwisho ofisini, nakumbuka sura ya allen na miwani yake akaniangalia na kunioneshea mkono wake kunijulisha kwamba mda umepita, nimechelewa tena. Siku hii sikuingia ofisini kwa bosi mapema, nikasubiri, lunch ikafika (walikua wanapika lunch ofisini) nikaenda kula. Niliporudi mezani nikaenda ofisini kwa bosi. Nilichofanya ni kumwambia kwamba, naomba aniongezee mshahara walau ufike laki 5, ili niweze kumudu maisha, nikiwa nafanya hii kazi. Sitosahau alichoniambia huyu mtu kwa ile lafudhi ya kiindi.

Bosi : Mic tumeongea hili jambo, fanya kazi kidogo, tutapanda mshahara kidogo kidogo huku mda unaenda, kazi tunapata nyingi tu, rudi kakae umeshamaliza zile website mbili nilizokupa jana? (Hapa hata machoni haniangalii)

Mimi: Bado, ndio nama…. (sijamaliza hata kuongea)

Bosi: Nenda kamalizie, tutaongea ukimaliza hizi. (AKAITA KWA NGUVU) ALLEN, EM NJOO HAPA MARA MOJA, UMESHATUMA EMAIL ZILE?
(mda wote huu hata machoni hajaniangalia, allen akaja, wakaongea kidogo kisha akaondoka, mimi bado nimekaa)

Bosi: Si unamuona allen hapa, amekaa miaka miwili anafanya kazi kwa bidii alianza kama wewe, leo mshahara wake ndio umefika hapo unapotaka.
(Nikawaza, hivi kila mtu analipwa mshahara sawa, haijalishi unachofanya ama?)

Mimi: naelewa hilo, ila mimi bila angalau laki tano siwezi fanya kazi hapa, itabidi niache (sikumbuki vizuri maneno niliyosema ila kitu kama hiki)

(Hapa bosi ndio akaacha kuangalia laptop yake na kunigeukia)

Bosi: Unajua mic, nimependa sana kazi yako, unajituma. Nataka tufanye kazi, tutafanya mambo makubwa sana.

Mimi: Nimekuelewa, na nataka kweli nifanye kazi hapa ila kwa laki 3 siwezi.
(Baada ya hii kupelekana mbele nyuma bila kwa dakika kadhaa, akakubali kongeza)

Bosi: Sawa Mic, tufanye basi kwa laki tatu na nusu…

Mimi: hapana Siwezi, laki tano ndio naweza endelea nayo
(baada tena ya dakika kadhaa mbele nyuma)

Bosi:Sikia michael mi nakuelewa, nmekuona toka ulipokuja siku ya kwanza kwamba na naelewa unapotoka, mi mwenyewe nilianzia hukohuko, nimeona kiatu chako unachovaa kinatobo, mi mwenyewe nilitembea sana kariakoo miaka ya 90 nikitafuta kazi, najiona mimi kwenye macho yako nilivyokua mdogo, ila leo nipo hapa, tufanye kazi tumalize tutaongea mbele. Sawa Nenda kakae, nitakulipa laki nne.

Mimi: (Nikawa nimechoka hata kuongea), Okay sawa.

Nikatoka hapo nikaenda kukaa kwenye meza yangu, allen na wenzake wote wananiangalia, kukawa kama kuna masaa matatu yamebakia ili tuondoke ofisini, mda wote huo nikawa nipo kwenye wakati mgumu, je niendelee na kazi maana nimepata nilichotaka, ongezeko la mshahara, ama niache kwa kua mshahara niliyoutaka sijapata. Nikasema nisubiri mda wa ofisi uishe jibu nitapata.

Allen na wenzake wakaondoka, mi nikawa wa mwisho kutoka, nikaenda ofisini kwa bosi sikumbuki ni kipi nilimwambia ila nikaacha kazi,ndani ya siku tatu. Nilijua elf mbili niliyokua nayo itanitosha kufika ofisini na kurudi, nikarudi ninapokaa enzi hizo also known as getto, elfu moja imekata hadi hapo, 500 nikaweka vocha nkabakia na 500. Kuna mangi ambae yupo karibu, nikaenda kukopa mkate siku ikaisha.

Uwoga uliniondoka, ndio point yangu. Sijui ningekua wapi kama ninge ngangana na hiyo kazi mwaka mzima, maana baada ya miezi minne hivi hadi sita nikapata kazi nyingine ambayo siyo ya hela nyingi ila ni kutoka kwa mtu mwenye akili sana za biashara, na aka nichallenge, hamna aliyesema kitu nikichelewa ofisini maana results nilizokua naonyesha ni za watu watatu, niliifanya hii kazi karibia mwaka.
Fast Forward mbele.. Mwaka 2015 nilipofanya ajira yangu ya mwisho, hauwezi amini nani ambae nilikutana nae. Allen. Sikumkumbuka, ila ye alinikumbuka, baada ya kuwaza, miwani yake amepiga, na saa mkononi huku amechomekea, akili ikajivuta na kumkumbuka.. akaniambia ameacha kazi pale baada ya miaka minne, na bora alivyoacha maana alikua ana nyonywa sana. Mtu mwingine nikakutana nae mwaka unaofuta akaniambia amefanya kazi kwa huyu “Bosi muhindi” kwa mwaka mmoja na hafai, na nina uhakika kuna watu ambao hadi leo bado wamekaa kwenye kazi ya huyu bosi muhindi kwa kua inabidi tu waingize kipato.
Mwaka 2017 – 2018 kwangu umekua wa kujifunza mambo mengi mapya ambayo yamebadilisha muelekeo wangu wa maisha, nimetafutwa na watu wengi sana kuweza endeleza mafunzo ya kupata kazi au ya kuanzisha biashara, na nitaendelea kuandika nitapo pata mda, ila kwa sahivi nakaribia kumaliza jenga application za kuweza ku tackle tatizo ambalo limeniumiza kichwa kwa mda mrefu sana, kujenga mfumo mpya kabisa ambao una value watu wanaofanya kazi kwa bidii. Nikirudi kwenye point ambayo nilianza nayo, ya jamaa wangu anaeendesha bajaji na bajaji yake mbovu miaka nenda, miaka rudi. Swali kubwa ambalo nakuaga nalo kila siku ni jinsi gani ya kumuonganisha mtu kama huyu kwenye opportunities ambazo zinaweza kumthamini uwepo wake wa kujali watu na kufanya kazi kwa bidii.
Nimekumbuka sana niliyopitia kwa kua nipo kwenye wakati mgumu kwa sahivi, je niendelee na vitu vinavyofanya kazi kwa kua vinasaidia kuendesha maisha, au nijaribu hii application kuendelea kuijenga ambayo ina uwezo wa kua kitu kikubwa sana na kubadili maisha siyo yangu tu, bali ya watu wengi sana wataoweza kupata nafasi kufanya kazi kwenye hii kampuni na watu watao tumia huduma ya application hii kwenye kazi zao. Uwoga unaniambia achana nayo, ni risk kubwa sana, haswahaswa unapozidi kukua na majukumu kuongezeka, uwoga unazidi kua mkubwa zaidi, maana sio mwenyewe tu sahivi, inabidi uwaze usalama wa familia na mengine, mda utaonyesha yote, kwa sahivi nipo kwenye maongezi na wawekezaji na bado njia haijajionyesha kwenda mbele.
Kuhusu mkwanzania.com na wapi itapoelekea kutoka hapa, nina mengi sana ya kuongelea na kuandika, nawaza niongeze videos na audio pia kwa mfumo wa podcasts, kuhusu project zangu, kufeli na kufanikiwa, ninayojifunza kila siku na mengine mengi,  na pia haya yote huku naelewa hali ya maisha kwa sahivi imebadilika, nawaza niachia kozi ile iliyokua ya kulipia iwe ya bure kabisa, huku natengeneza kozi nyingine ambayo itakua update ya vitu vipya baada ya mwaka mzima wa kozi ya kwanza kua hewani, nafuatilia njia nzuri ya kufanya hivyo, ahsanteni kwa wote wanaonitafuta ndio mnaonipa moyo kuendelea kuandika, na nitajitahidi kuiacha hii tovuti hewani kwa ajili ya yeyote ataetaka kujifunza.
Facebook Comments

Comments 0

Leave a Comment